SERIKALI imeruhusu mtu yeyote mwenye uwezo wa kuwekeza katika usafiri wa treni ajitokeze, ili kuuboresha.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Charles Tizeba, alieleza hayo mjini hapa
jana katika kongamano la uwekezaji Kanda ya Ziwa uliokuwa ukijadili
mambo mbalimbali yatakayoweza kunyanyua uchumi wa Kanda ya Ziwa kwa
kuzingatia sekta sita muhimu.
Moja ya sekta hizo ni ya uchukuzi ambao wawekezaji wa Kanda ya Ziwa
walieleza kuwa ili kuweza kunyanyua uchumi na kuvutia wawekezaji ni
lazima kuwepo na miundombinu mizuri ambayo ni viwanja vya ndege, treni
na barabara.
Akijibu hilo, Tizeba alisema ni kweli kuna changamoto katika
miundombinu Kanda ya Ziwa ikiwa ni pamoja na usafiri wa treni ambao
ungesaidia katika usafirishaji wa mizigo badala ya kutumia barabara
ambazo zina gharama kubwa huku akitolea mfano mtu anaweza kusafirisha
kwa sh milioni tatu badala ya milioni moja au 500,000.
Kutokana na hali hiyo, alisema serikali inaruhusu uwekezaji katika
njia ya treni kwa mtu kununua mabehewa ya abiria na mizigo na kufanya
mazungumzo na wizara tayari kwa kuanza kazi.
Hata hivyo alisema hadi ifikapo mwakani, serikali itakuwa
imeshaingiza nchini vichwa vya treni 13, locomotive 50, mabehewa mapya
ya abiria 274 na ya mizigo 990.
Hata hivyo, alisema hadi kufikia Juni kutakuwa na mabehewa mapya 22
ya mizigo na pia mabehewa 1,960 yatapatikana ndani ya miaka miwili ya
fedha ijayo.
Akizungumzia kuhusu usafiri wa ndege, alisema atahakikisha anasimamia upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza.
“Sio tu kuurefusha uwanja huo bali hata kutengeneza sehemu ya abiria,
tufanye marekebisho sehemu ya michoro, pia uendelezaji wa uwanja wa
ndege wa Bukoba na kwamba kwa sasa tani 50 zinatua na kuwepo na uwezo wa
kushusha abiria 70 kila siku,” alisema Tizeba.
Kongamano hilo litatilia mkazo uendelezaji wa sekta ya kilimo,
mifugo, uvuvi, maliasili na utalii, miundombinu, huduma za jamii na
nishati, sekta ambazo zina fursa nyingi katika Kanda ya Ziwa.
Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment