WATANZANIA wakiwamo wafanyabiashara wa viwanda,
kilimo na elimu, wametakiwa kujizatiti katika suala la uwekezaji kwenye Soko la
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), badala ya fursa hiyo kuwaachia raia wa
kigeni.
Kauli hiyo imetolewa mjini hapa juzi na Mkuu wa
Mkoa wa Mwanza, Injinia Evarist Ndikilo kwenye ufunguzi wa maonesho ya nane ya
biashara ya kimataifa, katika viwanja vya Nyamagana.
Alisema tayari Soko la Afrika Mashariki limeshaanza
kufanyakazi, hivyo ni vema Watanzania wakachangamkia fursa hiyo, kwa kuzalisha
bidhaa zenye ubora ili kuliteka soko hilo.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa wa Mwanza,
uzalishaji wa bidhaa zenye viwango vya kimataifa, ndilo jambo muhimu
linalotakiwa katika suala zima la ushindani.
“Tunapokuwa katika maonesho haya ya biashara ya
kimataifa, msisitizo wa serikali kwa Watanzania ni kuona wanachangamkia fursa
ya Soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Soko hili tayari limeshaanza kufanya kazi, kwa
hiyo tusije tukawa watazamaji kwa kuwaachia raia wa kigeni katika biashara hii.
Watanzania tuwekezeni na kutangaza bidhaa zetu zenye viwango,” alisisitiza RC
Ndikilo.
Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara
wenye Viwanda, Kilimo na Biashara (TCCIA), Mkoa wa Mwanza, Elibariki Mmari,
alisema maonyesho hayo yanazishirikisha nchi zote za Afrika Mashariki, China,
Singapore na Misri.
Aliiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuondoa
vikwazo mbalimbali katika maeneo ya mipakani, kwani kufanya hivyo itarahisisha
watu wengi kushiriki maonesho kama hayo.
Mmoja wa washiriki wa maonesho hayo, ambaye pia ni
Mkurugenzi wa Beijing China Shop, Celestin Patrick, aliiomba TCCIA kuandaa
uwanja mzuri wa maonesho, kwani Uwanja wa Nyamagana hauna hadhi nzuri.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment