Home » » JENEZA LA KICHANGA LAZUA BALAA!

JENEZA LA KICHANGA LAZUA BALAA!

                                     Jeneza likiwa na mwili wa mtoto
                                      Polisi wakiondoka na Jeneza kwa kuzika tena
                                           Kaburi la mtoto baada ya kuzikwa tena
JENEZA lenye mwili wa mtoto mchanga, limezua taharuki kwa wananchi na wakazi wa Mtaa wa Ihago, Kata ya Mahina, Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza. Tukio hilo la  kushangaza na la aina yake, lilitokea Agosti 29, mwaka huu, majira ya saa 12:00 asubuhi baada ya kugunduliwa na mfanyabiashara Ester Musa (28) likiwa limetelekezwa kwenye mlango wa mgahawa wake. Jeneza hilo linaaminika kufukuliwa na watu wasiofahamika kwenye moja ya makaburi eneo la Mahina jijini hapa.
 Akizungumza na gazeti hili kuhusiana na tukio hilo, Ester anayemiliki na kuendesha mgahawa alisema, alifika katika eneo lake hilo la biashara, ghafla akapigwa na mshangao baada ya kuona jeneza likiwa mbele ya mlango wa mgahawa wake.
“Nashindwa kujua nini maana ya tukio hili sababu hivi karibuni nilikuta barua imebandikwa ukutani ikinitaka nihame kutoka eneo hili, vinginevyo nitaona nitakachofanyiwa. Leo nimekuta jeneza mlangoni,” alisema Ester na kuongeza; Tukio hili nalihusisha na imani za kishirikina lakini kubwa linachangiwa na wivu wa kibiashara.Tangu lizaliwe sijawahi kuona jambo kama hili. Hapa sijawahi kugombana na mtu yeyote nashangaa kufanyiwa kitendo cha namna hii katika eneo la biashara yangu.”
 Mwenyekiti wa mtaa huo, Anthony Deus alisema kitendo cha kufukua mwili wa marehemu tena mtoto mchanga, si cha kibinadamu na ni tukio la kusikitisha katika jamii, hivyo watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.
Kaimu Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mwanza, ACP Christopher Fuime, alikiri kuwapo kwa  tukio hilo na kusema hakuna mtu aliyekamatwa akihusishwa nalo.
 “Tunaendelea na uchunguzi lakini hadi sasa hakuna aliyekamatwa akihusishwa na tukio hili la kusikitisha… wananchi wameuzika upya mwili wa mtoto huyo,” alisema.
 
chanzo:Globalpublishe

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa