Na John Maduhu, Mwanza
VIONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), waliokabiliwa na kesi ya kudharau amri ya mahakama, wamenusurika
kwenda jela miezi minne baada ya kufanikiwa kulipa faini.
Katika kesi hiyo namba 58 ya mwaka 2012, viongozi watano walikuwa wakikabiliwa
na kesi ya kudharau amri halali ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa
Mwanza, dhidi ya shauri namba 69.
Katika kesi hiyo, Wakili wa upande wa mlalamikaji, Boniphace Matata, alisema
viongozi hao walistahili kuhukumiwa kifungo jela kutokana na kudharau amri ya
mahakama ya kuwataka kufika ili kujibu tuhuma zinazowakabili.
Kesi hiyo ilifunguliwa na Diwani wa Kata ya Kitangiri, Henry Matata, aliyekuwa
akipinga uamuzi wa Kamati Kuu ya CHADEMA kumvua uanachama.
Katika kesi hiyo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Mwanza, Angelo
Rumisha, baada ya kusikiliza hoja za wakili wa mlalamikaji pamoja na utetezi wa
wakili wa walalamikiwa, aliwatia hatiani viongozi hao kwa kuwahukumu kifungo
cha miezi minne jela au kulipa faini ya Sh 155,000 kila mmoja.
Hata hivyo, viongozi hao walifanikiwa kulipa faini na kunusurika kwenda jela
kuanza maisha mapya ya miezi minne.
Walionusurika kwenda jela ni aliyekuwa Meya wa Jiji la Mwanza, Josephat
Manyerere, Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo Taifa, Benson Kigaila, Diwani
wa Kata ya Kirumba, Dan Kahungu, Katibu Uenezi wa Wilaya, Carlos Majora na
Katibu wa Wilaya ya Ilemela, John Anajus.
Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea mahakamani hapo Novemba 19, mwaka huu, na
walalamikiwa wote wanapaswa kuhudhuria mahakamani hapo bila kukosa.
Hivi karibuni, mahakama hiyo ilitoa hati ya kukamatwa kwa viongozi wa CHADEMA,
baada ya kudaiwa kudharau amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa
Mwanza.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment