Home » » Mfanyabiashara wa Kiasia auawa ‘kinyama’

Mfanyabiashara wa Kiasia auawa ‘kinyama’



 
Na John Maduhu, Mwanza
MFANYABIASHARA mwanamke mwenye asili ya Kiasia, Prazima Chande (60), ameuawa kinyama kwa kunyongwa na kisha kutobolewa macho na watu wasiofahamika akiwa nyumbani kwake.

Mfanyabiashara huyo aliyekuwa akimiliki Kampuni ya Uchapaji katika Kanda ya Ziwa ya Lake Printing, alikutwa na mauti hayo baada ya watu wasiofahamika kuingia katika nyumba aliyokuwa akiishi katika Barabara ya Kenyatta.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, mfanyabiashara huyo aliyekuwa akiishi peke yake katika nyumba hiyo, alikuwa akitarajiwa kusafiri Jumatatu ya wiki hii kwenda India kwa ajili ya mapumziko.

Taarifa hizo zimeeleza kuwa watu hao ambao bado hawajafahamika, walifika nyumbani kwa Prazima aliyekuwa akiishi peke yake baada ya mumewe kufariki miaka michache iliyopita na kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake kisha kutoboa macho yake. 

Hata hivyo, inadaiwa kuwa watu hao hawakupora kitu chochote katika nyumba aliyokuwa akiishi mfanyabiashara huyo, kwa madai kuwa sehemu iliyokuwa ikihifadhia fedha pamoja na vitu vingine ilikuwa ikifunguliwa na funguo maalumu.

Mfanyabiashara huyo, Jumatatu alifanyiwa mazishi kwa mwili wake kuchomwa moto katika makaburi ya Kihindu yaliyopo katika makutano ya mitaa ya Pamba na Kenyatta.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limesema bado halijapokea taarifa rasmi kuhusiana na tukio hilo na kueleza kuwa watatoa taarifa rasmi leo baada ya kupata taarifa rasmi juu ya tukio hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu, alisema bado hajapokea taarifa rasmi kwa kuwa jana Jumatatu ndiyo ameanza kazi rasmi mkoani Mwanza.

Hata hivyo, taarifa za uhakika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zimesema kuwa hadi sasa, jeshi hilo linamshikilia mmoja wa walinzi aliyekuwa zamu eneo la chini ya jengo alilokuwa akiishi mfanyabiashara huyo kwa ajili ya mahojiano zaidi juu ya tukio hilo.

“Tukio hilo lina utata mkubwa. Yule mama alikuwa akiishi ghorofani na Waasia wenzake, mlinzi yeye alikuwa eneo la chini, bado kuna utata mkubwa ndio maana polisi tunalichunguza kwa makini zaidi,” alisema mmoja wa polisi ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa