Na John Maduhu, Mwanza
WATU 65, wamenusurika kifo baada ya basi la
Kampuni ya Adventure walilokuwa wakisafiria kutoka Mwanza kuelekea Kigoma,
kuwaka moto na kuteketea.
Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kagera,
Philiph Kalangi, alisema basi hilo liliteketea moto jana saa nne asubuhi.
Kwa mujibu wa Kamanda Kalangi, tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha
Nyantakala, kilichopo mpakani mwa Mikoa ya Mwanza na Kagera.
Kamanda Kalangi alisema kuwa, basi hilo lenye namba za usajili T293 BBP,
lilikuwa likitoka Mwanza kuelekea mkoani Kigoma na kwamba liliwaka moto baada
ya kupata hitilafu katika mfumo wake wa umeme.
Alisema kwamba, baada ya kuanza kuwaka moto, abiria waliokuwamo walianza kutoka
nje kwa kutumia mlango wa kawaida pamoja na mlango wa dharura.
“Wakati wa tukio hilo, baadhi yao walipitia madirishani na wengine kwenye
milango kwa kuwa kila mmoja alikuwa akitaka kuokoa maisha yake,” alisema
Kamanda Kalangi.
Alisema kwamba, pamoja na abiria kufanikiwa kuokoa maisha yao, abiria tisa
walijeruhiwa vibaya katika harakati za kujiokoa na wamelazwa katika Hospitali
ya Wilaya ya Biharamulo kwa ajili ya matibabu.
"Ndugu mwandishi wa habari, hapa ninapozungumza nawe niko katika eneo la
tukio kabisa.
“Hili tukio ni baya sana kwa sababu hakuna mali au mzigo wowote uliookolewa,
yaani mizigo yote imeteketea kwa moto pamoja na vitu vingine walivyokuwa navyo
abiria kwa sababu walishindwa kushuka navyo kutokana na jinsi tukio lenyewe
lilivyotokea.
“Kwa hiyo, baada ya kutoka hapa, natarajia kwenda hospitalini kuwajulia hali
majeruhi na nadhani baada ya kumaliza mizunguko hii, nitakuwa katika nafasi
nzuri ya kutaja majina yao,” alisema.
Kuhusu abiria wengine walionusurika, alisema walitafutiwa usafiri mwingine na
kufanikiwa kuendelea na safari yao kuelekea mkoani Kigoma.
"Abiria wote wametafutiwa usafiri wa kuendelea na safari zao,
walichopoteza ni mizigo na vitu vingine, hakuna hata mmoja ambaye hakupata
usafiri wa kuelekea alikokuwa akienda,"alisema.
Mwakilishi wa Kampuni ya Adventure jijini Mwanza aliyejitambulisha kwa jina la
Ustaadh Juma, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema abiria
walionusurika walisafiri na basi jingine na kampuni hiyo lililokuwa likifuatana
na basi lililoungua.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment