Home » » WAMACHINGA MWANZA WAKANA KUMZOMEA PINDA

WAMACHINGA MWANZA WAKANA KUMZOMEA PINDA

Na John Maduhu, Mwanza


MUUNGANO wa wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama ‘wamachinga’ jijini Mwanza, umekanusha wanachama wake kuhusika na vurugu zilizopelekea kuzomewa kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, huku wakiwaonya baadhi ya wanasiasa kuacha kuhamasisha siasa za vurugu.

Kauli hiyo imetolewa jana na Makamu Mwenyekiti wa Muungano huo Said Tembo, walipokuwa wakizungumza na Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Baraka Konisaga, ambapo alisema kuwa vurugu hizo hazikufanywa na wanachama wake.

Tembo, alisema vurugu hizo zilifanywa na makundi ya wahuni wachache, ambao walikuwa wameandaliwa baada ya kunyweshwa pombe na mmoja wa wanasiasa.

Alisema kuwa, Muungano wao umefadhaishwa na kitendo kilichotokea cha kumzomea Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Pinda na kueleza kuwa, wanakilaani vikali na kutaka wahusika wote wachukuliwe hatua.

Tembo alisema kuwa, wao kama wafanyabiashara ndogo ndogo wanaotegemea biashara hiyo wasingeliweza kuandaa vurugu au kushiriki bali wangetumia fursa ya kuwepo kwa Waziri Mkuu kuwasilisha kero zao, ili Serikali itazame namna ya kuwasaidia.

"Hata katika mila na desturi kwa umri wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, sisi kama vijana hatungeliweza kumzomea, siasa zilipita kipindi kile na wananchi walifanya maamuzi ambayo tunayaheshimu, tayari tumeamua kukitumia kitengo chetu cha usalama kuisaidia polisi kuwabaini wahusika," alisema Tembo.

Naye, Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Baraka Konisaga alisema kuwa, anatarajia kukutana na wafanyabiashara wote ndogo ndogo kulingana na makundi yao, ili kujadili mambo mbalimbali muhimu kwa ajili ya kuwasaidia.

Alisema kuwa, wafanyabiashara hao wanapashwa kukataa kutumiwa na wanasiasa kwa ajili ya kuvuruga hali ya amani iliyopo katika wilaya ya Nyamagana.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa