na Jovither Kaijage, Ukerewe
BAADHI ya wakazi wa Wilaya ya Ukerewe, Mwanza wameishauri serikali kuachana na utaratibu wa kukimbiza Mwenge wa Uhuru kila mwaka ili kuepusha gharama zisizo za lazima kwa taifa.
Walitoa ushauri huo jana kwa nyakati tofauti wakati Mwenge huo wa Uhuru ulipopokewa na uongozi wa Mkoa wa Mwanza na kuanza kukimbizwa katika wilaya saba za mkoa huo.
Ainex Kagambirwe, alisema inasikitisha kuona fedha nyingi zinaendelea kutumika kugharamia utaratibu huo kila mwaka wakati Watanzania wengi wanakosa huduma muhimu kama matibabu na elimu bora.
Akieleza zaidi alisema fedha na rasilimali zinazogharamia mbio za Mwenge huo kila mwaka ni vema zikatumika kuboresha huduma za jamii ikiwamo ununuzi wa madawati na vifaa vingine shuleni, dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya na hospitalini.
Naye Mwalimu ambaye hakutaka jina lake litajwe mbali na kuunga mkono wazo hilo pia alishauri kuandaliwa utaratibu mwingine wa kukimbiza Mwenge kwa kupendekeza kiwepo kipindi maalumu cha kufanya zoezi hilo tofauti na sasa ambapo unakimbizwa kila mwaka na kuligharimu taifa fedha nyingi.
Alisema kama utawekwa muda maalumu wa kutekeza shughuli hiyo itasaidia kutengwa bajeti ya fedha za shughuli hiyo na kuondoa tatizo la muda mrefu la kutegemea michango ya kujitolea ambayo imegeuka kuwa kero kwa wananchi.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment