na Sitta Tumma, Mwanza
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza, kimemuonya Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje (CHADEMA), kikimtaka aache mara moja kutoa kauli za hovyo kwa lengo la kuwachonganisha viongozi wa Serikali na chama tawala.
Onyo hilo limetolewa juzi na Katibu wa CCM wilayani humo, Deogratias Rutta, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na kauli ya Wenje anayodaiwa kuitoa bungeni hivi karibuni, akimtuhumu Mkuu wa Wilaya hiyo, Baraka Konisaga, kuwa ametumwa na Rais Jakaya Kikwete kufanya kazi za kukiimarisha chama hicho.
Alisema, Wenje anatakiwa kujitambua kuwa ni kiongozi mwenye dhamana ya kuwatumikia wananchi kama alivyo mkuu wa wilaya, hivyo ni vema akaacha kutoa lugha ambayo si sahihi, kwani kufanya hivyo hapati sifa bali ni kupoteza sifa mbele ya jamii anayoiongoza.
Kwa mujibu wa katibu huyo, hivi karibuni CCM kilifanya maandamano makubwa yaliyojumuisha wananchi na wanachama wake, kulaani mgomo wa madaktari uliokuwa ukiendelea nchi nzima, kwamba walisikitishwa kumsikia Wenje akipotosha ukweli wa mambo bungeni.
”Kwanza Wenje siku hiyo ya maandamano hakuwepo. CCM inasikitishwa kumsikia akimuuliza swali la uongo Waziri Mkuu kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, alisema ametumwa na Rais Kikwete kuja kufanya kazi ya CCM.
”Pia huyu mbunge atambue kwamba yeye ni kiongozi wa wananchi kama alivyo mkuu wa wilaya. Sasa CCM inamuonya aache uropokaji, maana huko si kujenga sifa bali ni kujiharibia sifa mbele ya umma,” alisema katibu huyo.
Aidha, alisema kiongozi mzuri ni yule anayejitenga na mambo ya kusema uongo mbele ya jamii inayomzunguka, hivyo lazima Wenje na viongozi wengine wapime na kuheshimu kauli zao kabla ya kuzitoa hadharani.
Alisema kiongozi yeyote makini hawezi kutumia taranta na medani za siasa katika kuhadaa umma katika mambo ya uzushi, badala yake atalazimika kutumia busara na hekima pale anapohitaji kuuliza ama kusema jambo hadharani.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment