na Jovither Kaijage, Ukerewe
WATU sita wakiwemo viongozi watatu wa serikali ya Kijiji na Kisiwa kidogo cha Sizu, Kata ya Kagunguri, Wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza, wamehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 21 gerezani kila mmoja baada ya mahakama kuwatia hatiani kwa makosa mawili ya kujeruhi na kuiba mali.
Vingozi hao ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Sizu, Richard Msanyika (47), Mwenyekiti wa kijiji hicho, Balikoba Bihemo (46) na mwenyekiti wa kitongoji cha Ilundu A na Deus Isaya Nyamwelo (32).
Wengine ni Samson Maningi (21), Mkama Mahendeka (25) na Alex Edimund (42) wote wakazi wa kisiwa hicho cha Sizu.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Ukerewe, Reuben Luhasha, alitoa hukumu hiyo baada ya kuridhika pasipo shaka na ushahidi wa upande wa mashitaka kuwa watu hao walitenda makosa hayo.
Katika shitaka hilo ilidaiwa na mwendesha mashitaka wa Polisi, Inspekta Samwel Onyango, kuwa washitakiwa hao ambao kila mmoja alikabiliwa na makosa saba walitenda makosa hayo Mei 21 mwaka 2008 majira ya saa 1:00 asubui katika Kisiwa cha Sizu.
Aliendelea kuieleza mahakama hiyo kuwa washitakiwa hao kwa pamoja waliwashambulia na kuwajeruhi maofisa sita wa serikali waliokuwa katika shughuli ya kuzuia uvuvi haramu na kisha walichoma moto mtumbwi wao wenye injini na kusababisha hasara ya sh 3,930,000.
Aliwataja maofisa hao kuwa ni askari Polisi No. F. 8488 PC Hamza, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Murutunguru, Frotunatus Mtesigwa na Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Busagami, John Surus.
Wengine ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kameya, Steven Sindika, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Bugorola, Pius Mkama na Mwenyekiti wa kikundi cha kuhifadhi mazingira ya Ziwa Victoria (BMU’s) kituo cha Bugorola, Pascal Thomas.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment