na Sitta Tumma, Mwanza
DIWANI wa Igoma, Adam Chagulani (CHADEMA), amesema jumla ya sh milioni 60 zimetengwa kwa ajili ya kujenga barabara ya kutoka Hill Front hadi Kishiri katani humo.
Mbali na hayo, Chagulani amewaahidi wananchi wa Igoma ujenzi wa soko wa karibu na Sosoka, upimaji wa viwanja maeneo ya Kishiri na Bukaga lazima utekelezwe kwa wakati.
Diwani huyo alisema hayo juzi alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Igoma mjini, ambapo aliwaahidi wananchi yupo kwenye mchakato wa kujenga pia daraja la Fumagila, ili kuondoa kero inayowakabili.
“Napenda niwahakikishie wana Igoma kasi yangu ya kutekeleza miradi ya maendeleo inazidi kushika kasi. Kuna sh milioni 60 za kujenga barabara kutoka Hill Front hadi Kishiri.
“Ujenzi wa soko karibu na kwa Sosoka ramani yake imeshakamilika. Lakini tumepeleka madawati 120 sekondari ya Igoma, na tunatarajia kuweka umeme wa sola,” alisema.
Aidha, Chagulani alilazimika kuwaomba radhi wananchi wa kata hiyo kutokana na tofauti zilizoibuka kati yake na mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje (CHADEMA), na kusema tofauti hizo hazipo tena.
“Samahani sana wananchi wangu wa Igoma kwa tofauti zilizojitokeza kati yangu na Wenje. Uongozi wa CHADEMA taifa uliingilia kati na kutusuluhisha, na sasa hakuna tofauti tena,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment