Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina (mwenye miwani) baada ya kuwasili
kwenye kambi ya Uvuvi ya Kisiwa cha Galinzila leo na kuongea na wavuvi.
Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Estomiah Chang’a (mwenye kofia) na
kulia zaidi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ukerewe Frank Bahati
leo. Mhe. Mpina alichoma moto nyavu haramu za uvuvi zenye thamani ya
shilingi bilioni mbili.
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina (mwenye miwani) akiwahutubia
wavuvi kwenye kambi ya wavuvi katika kisiwa cha Galinzila Wilayani
Ukerewe ambapo baadaye alichoma moto nyavu haramu za uvuvi zenye thamani
ya shilingi bilioni mbili katika kijiji Kakukuru.
Umati
wa wavuvi kwenye kambi ya wavuvi ya Kisiwa cha Galinzila wilayani
Ukerewe wakimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina
(hayupo pichani) ambapo baadaye alichoma moto nyavu haramu za uvuvi
zenye thamani ya shilingi bilioni mbili katika kijiji cha Kakukuru
zilizokamatwa katika operesheni maalum ya siku tano ya kutokomeza uvuvi
haramu katika Wilaya ya Ukerewe leo.
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina akiwa katika picha ya pamoja na
kikosi kazi kilichofanya operesheni ya kutokomeza uvuvi haramu katika
Wilaya ya Magu na Busega mara baada ya kuteketeza kwa kuchoma moto zana
haramu za uvuvi zenye thamani ya Tsh 457,075,000/= katika kijiji cha
Kageye wilayani Magu leo.
WAZIRI
wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Luhaga Mpina ametaifisha na kuteketeza zana
haramu za uvuvi zenye thamani ya shilingi bilioni 2 zilizokamatwa wakati
zikitumika kwa shughuli za uvuvi katika visiwa vidogo vilivyopo ndani
ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza huku Shilingi milioni 120
zikikusanywa kama sehemu ya adhabu kwa wavuvi na wafanyabiashara
waliokutwa na zana haramu pamoja na makosa ya utoroshaji samaki na mazao
yake nje ya nchi.
Waziri
Mpina aliwaonya watu wanaotumia majina ya wavuvi kutishia kufanya
migomo isiyoisha na kuandamana baada ya uamuzi wa Serikali kuanza
kuchukua hatua stahiki za kudhibiti uvuvi haramu, na kwamba msimamo
uliowekwa na Serikali ni thabiti na usiyoyumba hivyo migomo na
maandamano ya watu wenye lengo la kukwamisha vita dhidi ya uvuvi haramu
haitasaidia chochote na badala yake operesheni kali isiyo na mwisho
itaendelea hadi pale uvuvi haramu utakapokoma ndani ya Ziwa Victoria.
“Rasilimali
zilizopo ndani ya ziwa hili ni mali ya wananchi sisi viongozi mliotupa
dhamana ya kuongoza kazi yetu ni ulinzi tu na endapo tutakomesha uvuvi
haramu nyie ndio mtakaonufaika hivyo ni itashangaza tajiri aliyempa
kibarua cha ulinzi, na mlinzi huyo akafanya kazi vizuri ya kulinda mali
za bosi wake alafu tajiri akamlalamikia kibarua wake sisi na watendaji
wa Serikali ni vibarua tu wenye mali ni ninyi hatua tunazochukua
zitaleta manufaa makubwa kwenu”alisema.
Pamoja
na kuteketeza zana haramu, Waziri Mpina alieleza hali ya upatikanaji wa
samaki aina ya sangara katika Ziwa Victoria ambapo alisema kwa mujibu
wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Samaki Tanzania (TAFIRI)
2017 unaonesha kuwa samaki waliochini ya sentimita 50 ni asilimia 96.6
hivyo samaki hawa ni wachanga na hawarusiwi kuvuliwa ambapo samaki walio
zaidi ya sentimita 85 ni asilimia 0.4 tu ambao ni wazazi na hawarusiwi
kuvuliwa pia. Samaki wa sentimita 50 mpaka 85 ambao ndio wanafaa
kuvuliwa ni asilimia 3 tu.
“Tafsiri
yake ni kwamba ziwa halina samaki wanaostahili kuvuliwa kulingana na
kasi ya uvuvi na pia samaki wazazi ni kidogo ambapo inatishia kumalizika
kwa samaki na shughuli za uvuvi kukoma katika Ziwa Victoria’alisema .
Akizungumza
kwa nyakati tofauti na maelfu ya wavuvi katika Visiwa vya Gagalini na
Kakukuru wilayani Ukerewe Waziri Mpina amesema hatua kali
zinazochukuliwa na Serikali dhidi ya uvuvi haramu hazilengi kuwaonea
wananchi wanyonge bali kuwatengenezea maisha bora ya kizazi cha sasa na
baadae ili kiweze kunufaika na rasilimali zilizoko ziwani.
Akiwa
katika eneo la Kakukuru Waziri Mpina alishiriki kuteketeza zana haramu
zikiwemo vyavu za Makila 14,103, Kokoro 188 , Nyavu za dagaa 211, Nyavu
za timba 450, Kamba za Kokoro 10,700 na ndoano 18,450 na Mitumbwi 109
zenye thamani ya sh. Bilioni 2.
Kaimu
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Uvuvi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mwaidi
Mlolwa amesema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kifungu cha 26
(i) (ii) kinamtaka kila mtanzania kulinda rasilimali za nchi yetu
ikiwemo samaki na mazao yake huku Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003
na Kanuni zake za mwaka 2009 zikikataza vitendo vya kutumia zana
zisizoruhisiwa kwa mujibu wa sheria.
Mkuu
wa Wilaya ya Ukerewe, Estomihn Chang'a alisema Serikali ya wilaya hiyo
itaendelea kuunga mkono juhudi za kupambana na uvuvi haramu na
kuwachukulia hatua stahiki kuwataka wananchi kuendelea kuwafichua wavuvi
haramu ili kulinda rasimali hiyo muhimu waliyopewa na Mungu.
Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Ukerewe , Frank Bahati alisema halmashauri
imewasimamisha kazi watumishi watatu kwa tuhuma za kujihusisha na uvuvi
haramu.Kwa upande wao baadhi ya wavuvi walimuomba Waziri Mpina
kuwasiliana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage ili kuona
namna ya kudhibiti nyavu zisizoruhusiwa kutengenezwa na kisha kuuziwa
wavuvi.
0 comments:
Post a Comment