Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto imesikitishwa na
tukio la mauaji ya watu saba wa familia moja waliokatwakatwa mapanga
baada ya kuvamiwa nyumbani, katika kijiji cha Sima wilayani Sengerema,
mkoani Mwanza, siku ya Jumatano usiku.
Wizara inalaani vikali mazingira
ya mauaji ya watu hao wa familia moja, ambapo wauaji walivamia nyumba ya
mama mjane na kumuuwa yeye mwenyewe, na watu wengine sita wakiwemo
watoto watatu.
Wizara inapongeza utayari wa
uongozi wa mkoa wa Mwanza na jeshi la Polisi amabo waliweza kufika
sehemu ya tukio ili kufuatilia mauaji hayo. Ni imani ya Wizara kuwa
Polisi kwa ushirikiano wa wananchi wa wilaya ya Sengerama wataweza
kuwasaka watuhumiwa wa mauaji na kuwachukulia hatua kali.
Wizara inawasisitiza wananchi
kutoa taarifa ambazo zitasaidia kuwamata watuhumiwa ili kuondoa hofu
miongoni mwa familia za kijiji cha Sima na wilaya ya Sengerema.
Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kutarejesha imani na utulivu miongoni mwa
wakazi wa Sengerema na hivyo kuweza kuendelea na shughuli zao za ujenzi
wa taifa.
Wizara inasisitiza kwamba kila
binadamu anayo haki ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha yake kwa
mujibu wa Sheria za nchi. Vitendo vya mauaji ya kikatili vinapotokea
katika familia zetu vinasababisha hofu kubwa miongoni mwa wanafamilia.
Mauaji hayo yanawakosesha amani wanafamilia na yanadhohofisha ari ya
ndugu wa familia kufanya shughuli zao kwa amani.
Wizara inaomba wanafamilia
waliopoteza ndugu zao kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki cha
majonzi makubwa, wakati Serikali ikiendelea na jitihada za kuwasaka
watuhumiwa wa mauaji hayo.
Erasto T. Ching’oro (Msemaji)
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
12/5/2016
0 comments:
Post a Comment