Home » » MADAKTARI,WAUGUZI MISUNGWI KUTUMBULIWA.

MADAKTARI,WAUGUZI MISUNGWI KUTUMBULIWA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 Imeandikwa na Mwandishi Wetu, Misungwi
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, kuwachukulia hatua kali ikiwamo kuwafukuza kazi wauguzi na madaktari, watakaokuwa wanawaomba rushwa wananchi jimboni kwake.
Kitwanga alisema amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wananchi kwa muda mrefu kuwa rushwa imekithiri katika Hospitali ya Wilaya jimboni humo na kuwakatisha tamaa wananchi wanaoenda kupata huduma hospitalini hapo.
Akizungumza huku akishangiliwa na mamia ya wananchi wa mjini Misungwi, Kitwanga alisema hali sasa imekuwa tete hivyo lazima hatua kali zichukuliwe kwa wale watumishi wachache ambao hawafuati sheria na kuweka mbele rushwa kwa wananchi.
“Ndugu wananchi madaktari na wauguzi ni watu muhimu sana katika jamii kwani wanatupa huduma nzuri kabisa, ila wataalamu hawa wanachafuliwa majina yao kwa watumishi wachache mno. Sasa tunataka kuwaondoa wale wachache ili tubaki na wengi ambao wanaipenda kazi yao, nawaonya wale wachache wenye tabia hiyo waiache haraka iwezekanavyo,” alisema Kitwanga ambaye pia ni Mbunge wa Misungwi.
Alifafanua kuwa ni kosa kwa daktari au muuguzi kumuomba rushwa mgonjwa au ndugu wa mgonjwa, kufanya hivyo ni hatari ni sawa na kuua, hivyo lazima sheria ifuate mkondo wake ili kulimaliza tatizo hilo sugu ndani ya Hospitali ya Wilaya na Misungwi kwa ujumla.
“Ndugu wananchi msiwe na wasiwasi kabisa, ninaaapa sitalivumilia tatizo hilo, na Mkurugenzi yupo hapa analisikia hili, hivyo lazima alifanyie kazi kwa kuwasimamisha kazi wauguzi au madaktari watakaotuhumiwa kuomba au kupokea rushwa,“ alisema Kitwanga.
Wakati huohuo, Kitwanga aliwataka wananchi hao kuanzisha vikundi ili waweze kupewa mikopo kupitia fedha alizoahidi Rais John Magufuli kuwa atatoa kwa kila kijiji Sh milioni 50.
“Fedha zipo jirani kuja, hivyo anzisheni vikundi ili muweze kukopeshwa fedha hizo na muweze kufanya mambo ya maendeleo, fedha hizo ni kwa ajili ya mikopo hivyo tumieni fursa hiyo kwa kuanzisha vikundi vyenu ili muweze kuzipata fedha hizo kwa uharaka zaidi,” alisema Kitwanga.
CHANZO: HABARI LEO.

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa