Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo ametoa siku mbili kwa
mwekezaji aliyejenga uzio wa maduka 41 katika shule ya msingi Sahara
katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza na uongozi wa shule hiyo kukaa kwa
pamoja na kuwasilisha kwake mpango kazi wa uwekezaji katika eneo hilo
kwa pande zote mbili.
Mulongo aliyasema hayo jana wakati alipokutana na wajumbe wa Kamati
ya Shule ya Msingi Sahara, watendaji wa Jiji la Mwanza na mwekezaji
aliyeingia mkataba wa miaka 33 na Jiji la Mwanza, Donald Kahema kujenga
uzio wa maduka 41 katika eneo la shule ya msingi Sahara.
Katika mkataba alioingia na Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Julai 15,
2008, Kahema ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Glowide Education Centre
ya jijini Mwanza, ametajwa kama mwekezaji na mpangaji wa maduka ya uzio
wa shule ya msingi Sahara.
Mulongo alisema uwekezaji uliofanywa katika eneo la Sahara, ambalo ni
muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa Jiji la Mwanza ni wa kutilia shaka kwa
madai kuwa ulilenga kuwanufaisha watu wachache wanaojificha kupitia
kwenye mgongo wa mwekezaji wa sasa. Alisema Serikali haiwezi kuvumilia
hali hiyo.
Awali Kahema ambaye ndiye aliyekuwa mwekezaji wa kwanza kuingia
mkataba na Halmashauri ya Jiji la Mwanza, anadaiwa kushindwa kukamilisha
ujenzi wa kipande kimoja cha uzio ambacho kilikabidhiwa kwa mwekezaji
mwingine kukijenga, huku mwekezaji huyo akilipa fedha kidogo kwa Jiji la
Mwanza.
Aidha, mwekezaji, Mwalimu Mkuu Shule ya Sahara Samike Gwanda na
wajumbe wa Kamati ya Shule walishindwa kutoa maelezo ya kina juu ya
taratibu zilizotumika kujenga uzio wa shule hiyo, ikiwamo kumchukua
mwekezaji mwingine, Michael Kisiki kujenga sehemu ya kipande cha uzio
huo, hali iliyokiuka taratibu za ujenzi.
Kwa upande wake, Kahema aliyeingia makubaliano ya kuwekeza katika
eneo hilo kwa muda wa miaka 33 kwa gharama ya Sh bilioni 1.6, alisema
alifuata taratibu na sheria za ujenzi wa uzio huo kwa kuandika barua kwa
uongozi wa shule hiyo na kupewa kibali na uongozi wa Halmashauri ya
Jiji la Mwanza.
CHANZO ; HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment