Home » » Wasira sasa ajivunia uzoefu.

Wasira sasa ajivunia uzoefu.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, amesema amechukua fomu kugombea urais ili kutumia uzoefu wake kusaidia nchi.
 
Alitoa kauli hiyo jana mjini hapa alipofika kutafuta wadhamini na kwamba uzoefu alionao unatokana na kufanya kazi katika serikali  zote tangu uhuru  hadi sasa ni nyenzo muhimu kwake kuwania nafasi hiyo kutokana na Taifa kwa sasa linahitaji mtu anayejua lilikotoka, lilipo na liendako.
 
“Nimefanya kazi  katika serikali zote hadi sasa, katika serikali ya Rais Kikwete amepangua na kupangua, lakini hakunipangua, nimekuwa Waziri wa Kilimo, Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri katika ofisi ya Rais na hivi karibuni kurudi Wizara ya Kilimo,” alisema na kuongeza:
 
“Kubaki katika nyadhifa zote hizo kwa muda wote ni ishara kuwa mimi nimekuwa na uwezo wa kufanya kazi na pia kumenisaidia kuijua nchi,” alisema.
 
Alisema kujua nchi sio kuijua mipaka bali ni pamoja na kujua maendeleo na matatizo ya wananchi kwa maelezo kuwa nchi ni watu.
 
“Nimeamua nitumie uzoefu wangu na elimu niliyopata kazini tena kwa muda mrefu nisaidie nchi katika kipindi cha mwaka 2015/20 kwa sababu mazingira ya sasa yanataka mtu anayejua tulikotoka, tulipo na tuendako,” alisema Wasira.
 
“Mimi ninajua tulikotoka mahali tulipo na nina ndoto ya tunakokwenda, na kama hujui tulikotoka huwezi jua tunakokwenda kwa sababu mtu asiyejua tulikotoka amekwishapotea maana akitaka kurudi hawezi kujua pa kurudi atarudi wapi?” alihoji.
 
Wasira alisisitiza kuwa uongozi wa nchi unahitaji busara na uzoefu wa kutosha kujua jambo namna lilivyo.
 
Mbele ya makada waliojitokeza kumdhamini, Wasira alitamba kuwa yeye ni msafi, hana kashifa na kwamba hakusudii kufanya jambo la kashfa.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa