Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Na Daniel Mbega, Mwanza
KESI
ya mauaji ya Aaron Nongo mwenye ulemavu wa ngozi (albino) imeanza
kusikilizwa tena leo hii kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza baada ya
kusimama kwa miezi takriban mitano.
Shauri
hilo namba 213 la mwaka 2014 liko mbele ya Jaji Robert Makaramba,
ambaye ndiyo kwanza ameanza kulisikiliza baada ya jaji wa awali, Ashery
Sumari, kupewa uhamisho.
Washtakiwa
katika kesi hiyo walikuwa watano, lakini leo hii mahakama imearifiwa
kwamba mmoja – Paulo Budeba Genji maarufu kama Lumalija – alifariki
dunia Novemba 22, 2014 katika Hospitali ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure,
wakati akiwa mahabusu.
Taarifa
hiyo ilitolewa na kiongozi wa mawakili wa upande wa mashtaka, Emil
Kiria, ambaye aliiomba mahakama, akirejea Kifungu cha 284 (a) cha Sheria
ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kwamba inapotokea hali kama hiyo
mashtaka dhidi ya mtu huyo yanafikia kikomo, ombi ambalo lilikubaliwa na
mahakama.
Washtakiwa
waliobakia kwenye kesi hiyo ni Chacha Jeremia, Mathew Jeremia Mlimi,
Paschal Lugoye Mashiku na Alex Joseph maarufu kama Bugwema Silola
Jangalu. Kesi
hiyo ambayo inaendelea tena kesho katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza,
iko katika hatua ya ushahidi ambapo shahidi wa sita wa upande wa
mashtaka atatoa ushahidi wake.
Leo
hii mashahidi wawili wametoa ushahidi wao na kufanya idadi ya mashahidi
waliokwishatoa ushahidi wao kufikia watano mpaka sasa. Marehemu
Nongo aliuawa Juni 26, 2009 majira ya saa tatu usiku akiwa nyumbani
kwake Ibanda Relini, jijini Mwanza ambapo wauaji hao walimkata usoni na
kisha kumkata miguu yake yote miwili na kutoweka nayo pamoja na meno
mawili ya mbele.
Chanzo Jiachie Blog
0 comments:
Post a Comment