Tone

Tone
Home » » WAZABUNI WA VYAKULA MASHULENI WATISHIA KUGOMA.

WAZABUNI WA VYAKULA MASHULENI WATISHIA KUGOMA.


Katika Mkoa wa Mwanza, wazabuni wa vyakula mashuleni wametishia kugoma kutokana na Serikali kushindwa kulipa deni la Sh milioni 800.
Baadhi ya wazabuni hao wameieleza MTANZANIA kuwa wamekuwa wakidai fedha hizo kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo, huku Serikali ikiwapa ahadi hewa.
Mmoja wa wazabuni anayetoa huduma katika shule za sekondari za Bwiru wasichana na wavulana, ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, alidai kuwa anadai Sh milioni 300 katika shule hizo baada ya kutoa huduma ya chakula.
Shule ya Sekondari Mwanza, iliyopo katika Wilaya ya Nyamagana inadaiwa na mzabuni kiasi cha Sh milioni 116, ambazo ameshindwa kulipwa kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo.
“Ni kweli tunadaiwa kiasi hicho cha fedha na mzabuni huyo, Serikali imeshindwa kutuma fedha za kuwalipa wazabuni hao kwa wakati, endapo watasitisha huduma hawa wanafunzi itabidi tuwarejeshe makwao,” alisema mmoja wa walimu wa shule hiyo kwa sharti la kutotajwa jina lake.
Shule nyingine ambazo zinadaiwa na wazabuni ni Sekondari ya Nsumba pamoja na Ngaza, ambapo taarifa za uhakika zinaeleza kuwa kwa ujumla wake zinadaiwa zaidi ya Sh milioni 300.
Ofisa Elimu Sekondari katika Jiji la Mwanza, Emmanuel Katemi, alisema hawezi kulizungumzia suala hilo kwa kuwa linashughulikiwa na Serikali.

CHANZO GAZETI LA MTANZANIA
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa