Tone

Tone
Home » » RIPOTI MAALUM: WAFUNGWA WAAGIZA NYAMA YA PORINI

RIPOTI MAALUM: WAFUNGWA WAAGIZA NYAMA YA PORINI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
“Mimi… (anataja jina lake) naomba anikopeshe laki mbili, kama hana anikopeshe hata 100,000 umweleze hali halisi, nahitaji ili inisaidie kwenye rufaa yangu. Ni muhimu sana…” Sehemu ya barua 
Katika tovuti hii wiki iliyopita tuliwaletea sehemu ya pili ya mfululizo wa Ripoti Maalumu kuhusu kubainika kuwapo kwa mtandao wa uhalifu unaowawezesha baadhi ya watu kuratibu matukio  ya uhalifu wakiwa gerezani katika mikoa ya Kanda ya Ziwa. Leo tunaendelea.
Wakati awamu ya tatu ya Operesheni Tokomeza Ujangili ikianza na juhudi za Serikali kupambana na uhalifu hasa ujangili zikiendelea, juhudi hizo zinakwamishwa na baadhi watendaji wasiokuwa waadilifu.
Habari za kiuchunguzi zinaonyesha kuwa, baadhi ya watuhumiwa hata wafungwa wameweza kufanikisha kukwepa kifungo kwa kuandaliwa rufani na baadhi ya watendaji wa Serikali wanaoshirikiana nao.

Katika moja ya matukio yaliyo mfano halisi, wafungwa wawili (majina tunayo) waliohukumiwa kifungo cha miaka 20 jela Desemba 23 mwaka jana kwa makosa ya ujangili, baada ya kukutwa na hatia ya makosa hayo mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Bunda, waliachiwa na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, baada ya kukata rufani na kushinda, mapema mwaka huu.
Wafungwa hao ambao ni wakazi wa Wilaya ya Serengeti, mkoani Mara awali walihukumiwa kifungo hicho. Taarifa za uhakika zinaonyesha kuwa wawili hao walishtakiwa kwa makosa matatu ikiwamo kuingia katika Hifadhi ya Serengeti eneo la Katemwaka, Februari 28 mwaka jana bila kibali. Wawili hao walikamatwa saa tano usiku wakiwa na pikipiki moja, sime, shoka na meno manne ya tembo kinyume cha sheria.
Hata hivyo, katika maelezo yao polisi chini ya Sheria ya Ushahidi ya Mwaka 1967, kifungu cha 58 CPA20. R.E, (2002) yaliyowasilishwamahakamani, washtakiwa hao walikiri makosa.
Uchunguzi wa gazeti hili umethibitisha mmoja wa wafungwa hao kufanya mawasiliano ya barua akiwa Gereza la Butimba. Katika moja ya mawasiliano hayo anamwelekeza jamaa yake akakope Sh200,000 ili zimepelekwe kwa mwanasheria mmoja wa Serikali ili amsaidie katika rufani yake.
“Mimi… (anataja jina lake) naomba anikopeshe laki mbili, kama hana anikopeshe hata 100,000 umweleze hali halisi, nahitaji ili inisaidie kwenye rufaa yangu. Ni muhimu sana…” inaeleza sehemu ya barua hiyo pichani.
Sehemu nyingine ya barua hiyo inaeleza:  “Jitahidi nipate hata laki mbili uende nayo kwa Steti Atoni, yaani Wakili wa Serikali atachukua. Aangalie atakavyofanya ili aniokoe.”
Mawasiliano hayo na ushirikiano walioupata kutoka kwa baadhi ya watendaji wenye dhamana ya kutunza sheria unatajwa kuwawezesha wafungwa hao kukata rufani Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza baada ya kutumikia  kifungo chao cha miaka 20 jela kwa miezi michache.
Taarifa zinaonyesha kuwa watu hao walihukumiwa kifungo hicho Desemba 30 mwaka 2013 na maombi ya rufaa yao yalikubaliwa na Mahakama ya Wilaya ya Bunda Januari 2 mwaka huu kabla ya kushinda rufani na kuachiwa huru Septemba 4 mwaka huu.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa warufani hao walishinda rufani hiyo dhidi ya Serikali kutokana na kinachoelezwa kuwa wakili aliyeiwakilisha Serikali kutopinga sababu za rufani.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa