Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na
Tiba Bugando (Cuhas), Mussa Mdede ambaye alitoweka katika mazingira ya
kutatanisha Juni 17, mwaka huu ameokotwa eneo la Busagara mkoani hapa
akiwa hajitambui.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino
Mlowola alisema jana kwamba baada ya kupatikana alipelekwa katika
Hospitali ya Rufaa Bugando na kufanyiwa uchunguzi na jana aliruhusiwa
kwenda nyumbani.
Mdede ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso), alitoweka Juni
17 muda mfupi kabla ya kurudisha fomu za kuomba kutetea nafasi yake ya
urais katika uchaguzi wa viongozi wa Serikali hiyo ambao ulipangwa
kufanyika Juni 29, chuoni hapo.
Imedaiwa kwamba alitekwa nyara kutokana na
ushawishi mkubwa wa kisiasa alionao chuoni hapo sambamba na kupingwa na
baadhi ya watu kutokana na msimamo wake wa kutetea wanafunzi wa elimu ya
juu nchini.
Tukio hilo lilisababisha viongozi wa Cuhas
kusitisha shughuli zote za uchaguzi ambazo zilikuwa zinafanyika chuoni
hapo hadi rais huyo atakaporejea.
Makamu wa Rais wa Cuhas, Atukuzwe Mordecai alisema
Mdede alipatikana jana saa sita mchana baada ya kuokotwa na watu wawili
ambao ni wafanyabiashara eneo la Busagara, huku akiwa hajitambui.
“Tulipata taarifa jana (juzi) jioni kutoka kwa
mama mwenye nyumba anapoishi. Hadi sasa bado hana kumbukumbu vizuri na
kwamba hatambui kitu gani kilitokea, lakini kiafya yupo salama.”
Waziri Mkuu wa Cuhas, Thomas Benjamini alishukuru wasamaria wema waliomsaidia Mdede.
Hata hivyo, taarifa kutoka kwa baadhi ya watu wa
karibu na mwanafunzi huyo zinadai kwamba Mdede amekuwa akitishiwa na
baadhi ya watu na kumtaka atoe tamko kuhusu mchakato wa Katiba Mpya
akiwa Mwenyekiti wa Tahliso.
Pia, taarifa hizo zinadai kuwa alishawahi
kutengewa kiasi cha Sh20 milioni na watu ambao walimtaka aache kuwa na
misimamo na kwamba awe upande wao kitu ambacho alikipinga na kukataa
fedha hizo.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment