Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399
Wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama
wamachinga wa jijini Mwanza, wakifanya vurugu ya kuziba barabara baada
ya mabanda yao yaliyokuwapo eneo la Makoroboi kuvunjwa na mgambo wa
Manispaa ya Jiji usiku wa kuamkia jana.Picha/Joel Maduka
Katika vurugu hizo ambazo mabomu ya kutoa machozi yalitumika kuwatawanya wamachinga, askari kujeruhiwa na watu kadhaa kutiwa mbaroni, zilidumu kwa takribani saa nane.
Polisi wa Kikosi cha Kutuliza ghasia wakitumia mabomu ya machozi, walipita mitaani wakipambana wamachinga hao ambao waliokuwa wakipinga kitendo cha askari wa jiji kubomoa vibanda vyao vya biashara.
Vurugu zilianza saa 12:00 asubuhi baada ya wamachinga kufika eneo la Makoroboi, maarufu kwa maduka ya nguo, na kukuta vibanda vyao vya biashara vikiwa vimevunjwa.
Kuona hali hiyo walivamia msikiti ulio jirani na eneo hilo na kutaka kuuchoma moto kabla polisi wa kutuliza ghasia hawajafika ka kurusha mabomu ya machozi kuwatawanya.
Maduka na masoko katikati ya jiji la Mwanza vilifungwa kwa siku nzima jana wakati polisi wakipambana nao wakipita mtaa hadi mtaa wakifanya vurugu.
Barabara za kuelekea katikati ya Jiji pia zilifungwa na wamachinga baada ya kuweka mawe, magogo na matairi ili kuzuia mabasi ya abiria kuingia katikati ya jiji.
Pamoja na polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kutumia mabomu kuwatawanya, wamachinga hao hawakujali na waliendelea kupambana na polisi huku wakiwarusha mawe.
Kituo cha mabasi cha Pansiansi katika barabara ya Kenyatta kilifungwa na wamachinga hao huku wakizuia magari ya abiria kutoka au kuingia katika kituo hicho.
Hadi saa nane mchana, polisi walikuwa bado wanapambana naona walisikika wakisema hawatasalimu amri mpaka watakaporudishiwa vibanda vyao na kuruhusiwa kufanya biashara katika eneo hilo.
Polisi waliweka vizuizi katika barabara zote kubwa za katikati ya Jiji ili kuzuia magari na waenda kwa miguu kwa lengo la kujaribu kuwadhibiti wamachinga ambao walikuwa wanajichanganya na wananchi wengine ili kuwapiga chenga polisi.
Mamlaka ya jiji la Mwanza inaendesha operesheni ya kusafisha jiji, ili pamoja na mambo mengine kuhakikisha kuwa wafanyabiashara ndogondogo wanaofanya kazi katika maeneo yasiyostahili wanaondolewa.
Mamlaka ya jiji imetenga maeneo kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo ndogo katika maeneo ya Sahara, Pamba Road, Kenyatta na Barabara ya Posta, lakini baadhi yao wamekataa kuhamia huko.
Mwenyekiti wa chama cha Wafanyabiashara ndogo ndogo, Joseph Samuel, alisema wamachinga waliofanya vurugu jana ni wakorofi tu na kwamba hawawakilishi chama chao.
Vurugu hizo zilisababisha kujeruhiwa kwa askari mmoja kutoka kikosi cha Zimamoto na Uokoaji.Baadhi ya watu walioshuhudia tukio hilo, walisema vurugu hizo zilianza saa 12:00 baada ya wamachinga’ kufika katika maeneo yao ya biashara na kubaini uharibifu mkubwa uliokuwa umefanywa na mgambo wa jiji ambao pamoja na mambo mengine, walitumia tingatinga kuvunja meza zao.
Inadaiwa kwamba mgambo waliendesha operesheni hiyo tangu alfajiri ya saa 11 kutokana na agizo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.Hata hivyo, baadhi ya watu waliohojiwa na NIPASHE kuhusiana na vurugu hizo wameonyesha kusikitishwa kwa madai kuwa ni ukiukwaji wa dhana ya utawala bora, kwa kuwa wamachinga hawakupewa taarifa mapema ili waondoke kwa hiari yao.
Habari zinasema kuwa mgambo hao waliokuwa wamefuatana na askari polisi na walifunga barabara za kuingia eneo la Makoroboi, huku wakiwa na gari maalum la askari wenye mabomu ya machozi ambayo yalifyatuliwa na kuathiri baadhi ya wapitanjia.
Inadaiwa kwamba kutokana na hali hiyo, machinga waliamua kuvamia ghala la jiji ili kudai mali zao, kitendo kilichosababisha mgambo wajifungie ndani ya ghala kuogopa mashambulizi.
Baada ya kudhibitiwa, machinga hao walirejea tena Makoroboi na kuamua kutekeleza kwa moto vipande vya meza na mbao zilizokuwa zimeharibiwa na mgambo.
Mkaguzi wa Zimamoto na Uokoaji ambaye pia ni Mkuu wa kituo jijini hapa, Augostine Magera, alithibitisha kuwapo kwa tukio la kujeruhiwa kwa askari wa jeshi hilo, Nelson Byarugaba.
Magera anayekaimu nafasi ya Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto mkoani Mwanza, alisema askari huyo ambaye ni dereva alipigwa jiwe shingoni na kupata jeraha.
Hata hivyo hali yake inaendelea vizuri baada ya kupatiwa huduma ya kwanza kituoni hapo.Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Robert Mwinamila, alisema ofisi yake imesikitishwa na unyama unaofanywa na viongozi pamoja na watendaji wa serikali kutokana na kukiuka haki za binadamu na utawala bora.
“Mimi ndiye nilimpigia simu mheshimiwa Wenje( Ezekiel Wenje- Mbunge wa jimbo la Nyamagana) kumjulisha kilichotokea leo asubuhi. Kwa ujumla zoezi hilo halikuwatendea haki wamachinga kwa sababu hawajashirikishwa,” alisema Mwinamila.
Alidai kwamba wamachinga katika eneo la Makoroboi wanafanya biashara kihalali kwa sababu wana kibali kilichotolewa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe.
Katibu wa wamachinga, Renatus Kaizirege, alisema kuwa zoezi hilo limetekelezwa kisiasa kutokana na shinikizo la Mkuu wa Mkoa na kwamba wanaopaswa kushughulikia suala hilo ni wataalamu wa Jiji la Mwanza kwa kushirikiana na wamachinga na siyo vinginevyo.
Diwani wa Kata ya Nyamagana, Bhiku Kotecha alikataa kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa yeye siyo msemaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Alipoulizwa kwa njia ya simu jana jioni, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Danford Kamenya, alisema alikuwa kwenye kikao na kwamba angetoa ufafanuzi baadaye; ingawa hata hivyo baadaye alipotafutwa hakupokea.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga, alipotafutwa alisema alikuwa kwenye kikao kwa ajili kujadiliana na watendaji pamoja na viongozi wengine na wilaya na mkoa kuhusiana na suala hilo.
Kamenya alisema operesheni ya kusafisha Jiji ilianza tangu Mei 17, mwaka huu na kuwa wamachinga walishapewa taarifa.
“Tulianza vizuri alfajiri, lakini wamachinga baadaye walifika na kuanza kufanya fujo, alisema Kamenya na kuongeza kuwa hakuna mali zilizoharibiwa kwa kuwa waliochokuwa wakikifanya ni kuondoa uchafu zikiwamo meza.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Baraka Konisaga, alipoulizwa, alisema wenye mamlaka ya kuzungumzia suala hilo ni Halmashauri ya Jiji.
12 WATIWA MBARONI
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Christopher Faime, alisema jana kuwa watu 12 wamekamatwa kuhusiana na vurugu hizo.
Faime amewaomba wafanyabiashara ndogo ndogo kutii sheria na mamlaka na kuhamia katika maeneo waliyotengewa.
WENJE AOMBA MWONGOZO
Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje, jana aliomba mwongozo bungeni kutaka Serikali isitishe operesheni ya kuwaondoa wamachinga inayoendelea jijini Mwanza.
“Muda huu ninapoomba mwongozo wako Msheshimiwa Spika, eneo la Makoroboi jijini Mwanza limechafuka, kuna operesheni inaendeshwa ya kuwaondoa wamachinga.
“Hali hii ikiendelea inaweza kusababisha vifo vya watu na upotevu wa mali zao,” alisema.
Alisema suala la wamachinga limemaliza maisha ya watu mwaka 2011 na mwaka 2012 na linapaswa kutafutiwa ufumbuzi makini.
“Suala la Machinga ni la kitaifa, limetokea Mbeya, Dar es Salaam, Iringa na sasa Mwanza,” alisema na kuongeza karibu miji yote.
Alisema maduka yote jijini Mwanza yamefungwa, hakuna biashara inayoendelea na katika maana hiyo serikali itakuwa inakosa mapato na hata wananchi kukosa huduma na mapato pia.
Baada ya kuomba mwongozo huo kwa Spika, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema suala hilo linashughulikiwa.
“Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ametoka hapa, anaendelea kuchukua, ameenda kuwasiliana na Mwanza ili kujua nini kinaendelea huko.“Amekuja tu kupiga kura hapa, anaendelea na hatua zitachukuliwa,” alisema Lukuvi
Imeandikwa na Juma Ng’oko, Rose Jacob, Mwanza na John Ngunge, Dodoma.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment