Home » » Dengue yapiga hodi Mwanza, Mbeya, Dodoma

Dengue yapiga hodi Mwanza, Mbeya, Dodoma

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,Dk. Seif Rashid.
 
Ugonjwa wa homa ya dengue umepiga hodi katika baadhi ya mikoa ikiwamo Mwanza, Dodoma na Mbeya huku Dar es Salaam wagonjwa wakiongezeka.
Kaimu  Mkuu  wa Mkoa wa Mwanza, Baraka  Konisaga, alisema mtu mmoja  mkazi wa Kilimahewa Manispaa ya Ilemela amelazwa     katika Hospitali ya Rufaa ya Sekou-Toure tangu juzi baada ya kupimwa na kubainika anaugua  ugonjwa huo.

Kwa mujibu  wa Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Valentino  Bangi, mara  ya kwanza   mgonjwa huyo alifika hospitalini  hapo Mei 20,  mwaka huu na kupimwa damu huku  akilalamika kwamba anasumbuliwa na homa.

Aidha, Dk  Bangi alisema mkoa wa Mwanza  umeshapokea vitendanishi (vifaa kwa ajili ya kupima  damu) na umeanza kuweka hadhari  kubwa dhidi ya ugonjwa huo.

Katika Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam jana wagonjwa waliongezeka wanane ambao walitibiwa na kuruhusiwa, kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Faustinias Ngonyani.

Kwa mujibu wa Afisa Uhusiano Manispaa ya Temeke, Joyce Msumba, Hospitali ya Temeke wameongezeka wagonjwa wapya wawili.

Katika hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wagonjwa waliokuwa wamelazwa ni wanne na mmoja aliruhusiwa jana kwa mujibu wa  Afisa Habari wa hospitali hiyo, Aminiel Eligaesha.

Kaimu Dk. Kiongozi wa Hospitali ya Amana, Gilbert Ngua, alisema wagonjwa wanaougua ugonjwa huo ambao bado wamelazwa ni tisa, wanawake sita na wanaume watatu.

Naye Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja, alisema ugonjwa huo uimengia katika mikoa ya Mwanza alipogundulika mgonjwa mmoja, Mbeya wawili na Dodoma mmoja.

Mwamwaja alisema taarifa zinaonyesha kuwa Dar es Salaam hadi jana wagonjwa wa homa hiyo waliothibitika ni 43, wanne kutoka Ilala, Kinondoni 27 na Temeke 12 waliolazwa ni 15.

Imeandaliwa na Juma Ng’oko, Mwanza; Jimmy Mfuru, Hussein Ndubikile, Samson Fridolin na Elizabeth Zaya, Dar  
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa