Tarehe
27 Septemba ya kila mwaka ni Siku ya Utalii Duniani ambapo sherehe hizi
hufanyika duniani kote. Mwaka huu, Siku ya Utalii Duniani kitaifa
iliadhimishwa Jijini Mwanza ambapo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Mhe Lazaro Nyalandu alikuwa mgeni rasmi.
Mhe Lazaro Nyalandu akiweka saini kitabu cha wageni baada ya kufungua rasmi ofisi mpya ya Bodi ya Utalii Tanzania Kanda ya Ziwa
Mhe. Lazaro Nyalandu akipata maelezo kutoka kwa mtumishi wa Marine Parks and Reserves
Mhe. Lazaro Nyalandu akifurahia taswira ya mnyama aina ya simba aliyekuwa katika banda la Wizara ya Maliasili na Utalii
Maadhimisho haya yalipambwa na shughuli mbalimbali ikiwemo ufunguzi wa ofisi
mpya ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Kanda ya Ziwa. Ofisi hii
imefunguliwa ili kukidhi mahitaji ya utangazaji wa utalii kwa Kanda ya
Ziwa. Aidha, shughuli nyingine kuu ya ofisi hii ni kuhamasisha utalii
kwa wananchi wa Mwanza na pia kuanisha vivutio vipya ya utalii na
kuvitangaza.
Mhe Lazaro Nyalandu akipata maelezo kutoka mtumishi katika banda la Wizara ya Maji
Akizungumza katika kilele cha Siku
ya Utalii Duniani, Mhe Lazaro Nyalandu aliwaasa wananchi wa Mkoa wa
Mwanza kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya utalii na kushangaa
nchi yao. Akitumia maneno yaliyomo kwenye wimbo wa ‘Nakupenda Tanzania’
yasemayo “Tanzania Tanzania ninapokwenda Safarini, kutazama maajabu”
alisema wimbo huu uliotungwa na wazee wa zamani ulionyesha hazina kubwa
ya vivutio vilivyopo nchini na hivyo kuhamasisha utalii kwa wananchi
wote.
Mhe Lazaro Nyalandu akiangalia kazi za mikono ya kikundi cha utamaduni kutoka Mugumu.
Sherehe hizo pia
zilipambwa na burudani ya ngoma za asili kutoka kikundi cha utamaduni
cha Bujora. Pamoja na ngoma hizo, mabanda yaliyofanya vizuri katika
maonyesho haya yalizawadiwa ambapo Wizara ya Maliasili na Utalii
illibuka mshindi wa kwanza, ikifuatiwa na Wizara ya Maji na ya tatu
ilikuwa Hoteli ya J.B.Belmont ya Jijini Mwanza.
Wengine
waliozawadiwa ni wanafunzi wa shule ya sekondari ya Kirumba waliofanya
vizuri katika mashindano ya insha inayohusu utalii. Washindi hao ni
Zuberi Kihumbe wa Kidato cha Pili, wa pili ni Mariam Shabani wa Kidato
cha Pili na wa tatu ni Renatus Leonard wa Kidato cha Tatu.
Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii, Mhe Lazaro Nyalandu alitoa rai kwa wananchi
kuwekeza kwenye sekta ya utalii kwani takwimu zinaonyesha kuwa kati ya
kazi kumi duniani moja ina uhusiano wa moja kwa moja na utalii.
Aliwashauri kuitumia ofisi ya TTB ili kujielimsha juu ya fursa
mbalimbali za utalii zinazopatikana Kanda ya Ziwa.





0 comments:
Post a Comment