Home » » Kanisa latakiwa kumaliza tofauti

Kanisa latakiwa kumaliza tofauti




UONGOZI na baadhi ya waumini wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Victoria Nyanza (DVN), jijini Mwanza, wameshauriwa kumaliza tofauti zao na badala yake washirikiane kuimarisha amani na upendo.
Ushauri huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na Askofu Mkuu wa Kanisa la African Inland Tanzania (AICT), Silas Kezakubi, alipokuwa akihitimisha misa ya Jubilee ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Dayosisi ya DVN.
Alisema siku zote migogoro haijengi badala yake inabomoa, hivyo ni vema ukawepo ushirikiano wa pamoja katika kulijenga kanisa.
“Niliwahi kusikia migogoro hapa. Vitu hivi huwa vinajitokeza, lakini nawaombeni Wakristo wenzangu imarisheni ushirikiano wa kutakasa ufalme wa Mungu,” alisema Askofu Kezakubi.
Pamoja na hayo aliushauri uongozi wa kanisa hilo kubuni mradi wa jengo kubwa lenye ghorofa litakalokidhi mahitaji ya huduma za Mungu, na kwamba yeye binafsi atachangia sh 500,000 katika ujenzi huo.
Pia aliwaomba viongozi wote wa Kikristu kuondokana na utegemezi wa fedha kutoka kwa wafadhili na badala yake walihudumie kanisa kwa nguvu na maarifa yao waliyopewa kutoka kwa Mungu.
Awali, Askofu Mkuu wa Kanisa la DVN, Boniphace Kwangu, aliwaomba waumini kuunganisha nguvu kulijenga kanisa hilo.
Chanzo: Tanzania Daima


0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa