Home » » JIJI LA MWANZA LAGEUKA KUWA UWANJA WA KIVITA! NI BAADA YA MAPAMBANO MAKALI KATI YA POLISI NA WALIODHANIWA KUWA MAJAMBAZI

JIJI LA MWANZA LAGEUKA KUWA UWANJA WA KIVITA! NI BAADA YA MAPAMBANO MAKALI KATI YA POLISI NA WALIODHANIWA KUWA MAJAMBAZI




na Sitta Tumma, Mwanza


JIJI la Mwanza juzi liligeuka kuwa uwanja wa kivita, baada ya kutokea mashambulizi makali ya risasi baina ya askari polisi na kundi la watu wanaodhaniwa kuwa majambazi yaliyokuwa yakijihami kwa silaha za kivita.
Taarifa zilizoifikia Tanzania Daima Jumatano kutoka eneo la tukio zinaeleza kwamba mashambulizi hayo yaliyodumu kwa takribani dakika kumi yalitokana na kundi hilo la majambazi kutaka kuvamia kituo cha mafuta cha GBP, kilichopo kando kando ya barabara ya Kenyatta, Igogo jijini Mwanza majira ya saa mbili usiku.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, na Naibu Kamishna Ernest Mangu alithibitisha kutokea kwa tukio ambalo inaaminika majambazi hao walikuwa na silaha nzito za kivita. Majambazi watatu waliuawa katika mapambanao hayo.
Alisema polisi walipata taarifa za siri kutoka kwa raia wema dhidi ya majambazi hayo, na walifika eneo la kituo hicho cha mafuta kisha kuyakuta majambazi hayo yakijiandaa kuvamia.
Katika maelezo yake kwa waandishi wa habari, Kamanda Mangu alisema majambazi hayo yalilazimika kujibu mapigo ya polisi kwa kutumia silaha nzito za kivita aina ya SMG na kufanikiwa kuwaua watatu na wengine wakikimbia kusikojulikana.
“Idadi halisi ya majambazi haijafahamika hasa. Maana yalitokea majibizano makali ya risasi. Lakini askari walikuwa makini na wakafanikiwa kuyaua matatu na mengine yakakimbia,” alisema Kamanda Mangu.
Alisema katika mapambano hayo polisi walifanikiwa kukamata bunduki moja aina ya SMG yenye namba za usajili 2916 pamoja na risasi saba, na kwamba taarifa walizonazo majambazi hayo yanatoka Wilaya ya Ngara mkoani Kagera.
“Baada ya majibizano makali ya risasi, katika eneo la tukio yaliokotwa maganda ya risasi 22. Miili ya hawa jamaa imehifadhiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando,” alisema.
Kufuatia tukio hilo, Kamanda Mangu ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za siri kwa jeshi hilo dhidi ya wahalifu ili wahusika waweze kudhibitiwa kwa mujibu wa sheria.
Katika tukio jingine, watu wasiojulikana wameteketeza kwa moto nyumba tisa za nyasi za familia moja, katika Kijiji cha Nyehunge wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
Kamanda Mangu alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 11, mwaka huu majira ya saa 10 na 12 jioni, na chanzo cha tukio hilo kinadaiwa ni imani za kishirikina.
“Kuna kijana Severine Renatus (14), mwanafunzi wa darasa la saba Shule ya Msingi Nyehunge alipotea kwa muda wa siku nne.
“Baada ya kupatikana kwa mwanafunzi huyo na kuhojiwa na wazazi wake, alisema alifichwa kwenye nyumba hizo, ndipo wazazi walipotoa taarifa kwa sungusungu wa kijiji hicho, ambao waliamua kukusanyika na wanakijiji wengine kisha kwenda kwenye nyumba hizo, na wenye nyumba hizo waliamua kukimbia,” alisema Kamanda Mangu.
Hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo, lakini polisi wanaendelea na upelelezi. 

CHANZO: DAIMA

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa