Na John maduhu, Mwanza
SERIKALI
imeombwa kutazama upya au kufuta ushuru wa vifaa vya maabara, ili viweze
kupatikana kwa urahisi na kuwawezesha wanafunzi kusoma kwa vitendo.
Ombi hilo lilitolewa na Mkuu wa Shule ya Sekondari Sunrise, Zacharia Machumu katika mahafali ya tano ya shule hiyo, yaliyofanyika jana jijini hapa.
Machumu alisema, shule nyingi zimekuwa zikishindwa kumudu gharama za kununua vifaa vya maabara, kutokana na ushuru mkubwa wa kuingiza vifaa hivyo na kusababisha bei kupanda.
Alisema kwa kuwa Serikali iko katika mipango madhubuti ya kuhakikisha wanafunzi wanasoma masomo ya sayansi kwa ajili ya taifa kuwa na wanasayansi wengi siku zijazo.
“Ni wakati mwafaka sasa kwa Serikali kuondoa ushuru wa vifaa vya maabara, ili kuwawezesha wanafunzi wengi wanaopenda kusoma kwa vitendo.
“Wanafunzi wengi wamekuwa wakishindwa kuendelea kusoma masomo ya sayansi kutokana na kukabiliwa na uhaba wa vifaa vya maabara, Serikali ichukue hatua,” alisema Machumu.
Akizungumzia maendeleo ya shule hiyo, mkuu wa shule hiyo alisema, tangu shule hiyo ianzishwe mwaka 2006, imekuwa ikifanya vizuri katika mitihani ya taifa.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment