Wanafunzi wa shule ya msingi Katende kisiwani Ukara, Wilaya ya Ukerewe wakisomba matofali wakati wa saa za masomo (picha na Jovither Kaijage)
Jovither Kaijage – Ukerewe
BARAZA la madiwani la halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Mwanza limetaka kukomeshwa vitendo vya kutumikisha wanafunzi kama watumwa kwa lengo la shule hizo kujipatia fedha za kuchangia ziara za mwenge wa Uhuru.
Baraza hili limetoa msimamo huo jana katika kikao cha kawaida cha baraza hilo ambapo pamoja na mambo mengine pia ilitolewa taarifa ya shughuri za maendeleo zilizotekelezwa katika mwaka wa fedha wa 2011/012.
Wakichangia taarifa ya kamati ya elimu, afya na maji baadhi ya madiwani walitaka idara ya elimu kuacha kuchangisha fedha katika shule za msingi kwasababu michango hiyo ni chanzo cha wanafunzi kutumikishwa hasa kwa kusomba mawe na matofari.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Pius Matome alisema uchunguzi uliofanywa na kamati yake umebaini kuwa kila shule ya msingi katika wilaya hiyo inatakiwa kutoa mchango wa sh. 20,000 kwaajiri ya Mwenge wa uhuru .
Alisema mchango huo pamoja na mingine inayoelekezwa na idara ya elimu imesababisha walimu kutumia wananfunzi kufanya vibarua ili zipatikane fedha za kutoa michango hiyo.
Alisema pia uchunguzi huo umebaini kuwa hali ya kifedha katika shule za msingi katika wilaya hiyo ni mbaya kwasababu fedha ya matumizi ya kawaida iliyopelekwa shuleni katika kipindi cha fedha cha mwaka uliopita ni ndogo ambapo kila mwanafunzi amepata sh. 2,000 badala ya sh. 10,000 kama sera ilivyo.
Akieleza zaidi tatizo hilo amesema vitendo hivyo mbali ya kukiuka sera ya elimu na sheria za ajira pia linasababisha wanafunzi kutumia muda wa masomo kufanya kazi hizo hali ambayo inaathiri taaluma na maendeleo ya wanafunzi.
Afisa elimu ya msingi wa wilaya hiyo, Fidelis Munyogwa amekiri kuwa kila shule imeombwa mchango huo kwaajiri ya shughuri za mwenge wa uhuru lengo likiwa ni kuiwezesha jamii kundelea kuenzi utamaduni wa nchini yetu.
0 comments:
Post a Comment