Home » » MTUMBWI WAUA WATATU

MTUMBWI WAUA WATATU


na Jovither Kaijage, Ukerewe
WATU watatu wamefariki dunia katika Wilaya ya Ukerewe, Mwanza baada ya mtumbwi wao kupigwa na dhoruba na kuzama katika Ziwa Victoria.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Leberatus Barlow, alisema kuwa, mtumbwi huo ulikuwa umebeba watu 15 ambao kati yao watatu walifariki dunia, na 12 waliokolewa na wavuvi waliokuwa karibu na eneo hilo.
Barlow aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Mgalla Yustinian (55), Pascazia Lyaganga (55) wakazi wa Kijiji cha Buzegwe na Nyanjala Dotha (45) ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Bukongo.
Mkuu wa wilaya hiyo, Mary Tesha, alisema watu hao walikumbwa na mkasa huo juzi jioni wakati wakitoka Kijiji cha Buzegwe kwenda kisiwa cha Kweru kuani msiba wa ndugu yao.
Na, Diwani wa Kata ya Kagunguri, Misana Ghatawa, alisema watu hao ambao walipata mkasa huo muda mfupi baada ya kuondoka katika mwalo wa Ilondo, miili yao imepatikana na kuchukuliwa na ndugu zao kwa ajili ya mazishi.
Baadhi ya wavuvi walioshuhudia tukio hilo walisema mtumbwi huo ulioonekana umeelemewa, ulizama baada ya kupigwa na mawimbi makubwa katika Ziwa Victoria.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa