Home » » WANANCHI WAUA WATATU KWA TUHUMA ZA WIZI

WANANCHI WAUA WATATU KWA TUHUMA ZA WIZI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WATU watatu wanaodhaniwa kuwa ni vibaka wameuawa na wananchi wenye hasira kwa tuhuma za kuendesha uporaji kwa kuvunja nyumba za watu na kuiba.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentine Mlowola jana alithibitisha kutokea kwa tukio hilo la kuuawa kwa watu hao wanaodaiwa kufanya uhalifu kwenye mitaa mbalimbali ya kata ya Buswelu usiku wa manane.
Watu hao ambao walikuwa zaidi ya wanne wanatuhumiwa kufanya uhalifu katika matukio matatu tofauti ambapo katika mtaa wa Isela walibomoa madirisha mawili na kuingia kwenye nyumba kisha kuiba Sh 260,000.
Aidha walihamia mtaa mwingine kama mita 300 kutoka kwenye nyumba ya awali na kubomoa mlango kwa kutumia jiwe kubwa maarufu kama ‘fatuma’ na kisha kuingia ndani na kuiba Sh 50,000.
Katika tukio la tatu walivunja nyumba nyingine kwa jiwe la fatuma na kisha kupora simu ya mkononi.
Alisema wananchi walianza kupeana taarifa juu ya matukio hayo, ndipo walipoanza kuwafuatilia na kwa kuwa walikuwa wakitumia pikipiki na mvua ilikuwa imenyesha walishindwa kukimbia sana hivyo wananchi walifanikiwa kuwakamata.
Waliouawa katika tukio hilo ni pamoja na Nestory Cosmas, Richard Manyiruzi na mwingine aliyetambulika kwa jina moja la Safari wenye umri wa kati ya miaka 20 na 30 na wakazi wa mtaa wa Nyamandoke.
Watu hao waliuawa na wananchi kwa kutumia silaha za jadi na kwamba miili yao imehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya Bugando na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi.
Chanzo:Habari leo

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa