Tone

Tone

WALIMU WAPYA WAANDAMANA MWANZA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
ZAIDI ya walimu 50 kutoka shule mbalimbali za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Manispaa ya Nyamagana mkoani hapa, jana waliandamana hadi ofisi za mkurugenzi wa halmashauri kushinikiza kulipwa mshahara wa mwezi uliopita.
Mbali na kudai mshahara, walimu hao pia wanataka kulipwa fedha walizotumia kwa ajili ya nauli wakati wa kuripoti kazini.
Hii ni mara ya pili walimu hao kuandamana, kwani Mei 6 mwaka huu waliandamana wakitaka walipwe madai yao na kutishia kutoingia madarasani.
Tanzania Daima ilishuhudia walimu hao wakiwa wamekusanyika nje ya ofisi za halmashauri ya jiji, wakisubiri kukutana na mkurugenzi, Halifa Hida, ambaye inadaiwa awali alikuwa safarini kikazi.
Walimu wanaituhumu ofisi ya halmashauri ya jiji kwa uzembe kwa sababu wenzao walioajiriwa pamoja katika Manispaa ya Ilemela wameshalipwa mishahara na madai yao mengine.
Habari zimedai kuwa ni walimu 43 pekee ndio wamelipwa mishahara kati ya 164 waliopangiwa kufanya kazi katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza, mwanzoni mwa mwaka huu, na kwamba wamekuwa wakielezwa kuwa majina yao yako wizarani, ambako yalitumwa kabla ya Aprili mwaka huu kwa ajili ya uhakiki.
Ofisa mmoja wa halmashauri hiyo aliliambia Tanzania Daima kuwa walimu hao wanadai zaidi ya sh milioni 80, na kwamba awali baada ya kuona wamecheleweshewa mishahara yao, walitaka wakopeshwe fedha ili waweze kujikimu wakati wakiendelea kusubiri.
Akizungumza kwa sharti la kutotaja jina, afisa huyo alisema uongozi wa jiji ulidai hauna fedha, na badala yake ukawatuma kwa walimu wakuu katika vituo vyao vya kazi ambao pia walisema hawana fedha za akiba kwa ajili ya kuwakopesha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Hida, hakuwa tayari kuzungumzia jambo hilo licha ya kufuatwa. 
Chanzo;Mwananchi

KKKT WATOA TAMKO KANISA LA MWANZA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria (DMZV), limeitaka Serikali kuhakikisha inawatafuta watu waliohusika na tukio la bomu lililolipuka kanisani hapo juzi.
Pia, limewataka Wakristo kuwa watulivu, wasiogope wala wasitishwe na mashambulizi hayo na kwamba wasilipize kisasi.
Akizungumza kwenye Kanisa la Imani Makongoro Misheni jana, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki Ziwa Victoria, Andrew Gulle alisema wanaamini shambulio hilo ni la kigaidi na kwamba, Serikali inapaswa kuchukua hatua ya kuwasaka wanaohusika.
“Kanisa tunaamini tukio hili linahusiana na ugaidi, umefika wakati Serikali ikachukua hatua za kuwasaka waliohusika ili sheria ifuate mkondo wake,” alisema Gulle.
Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya dini wanasema huenda tukio hilo linatokana na migogoro inayoendelea kanisani hapo kwa sababu tayari kuna baadhi ya waumini wamejitenga kwa kuanzisha kanisa lingine.
“Wasikwepe matatizo yao ya ndani, kuna askofu aliuawa kwa kupigwa tofali kutokana na migogoro, hivyo hata hili (tukio) litakuwa ni migogoro inayoendelea,” alisema mmoja wa waumini ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Askofu Gulle alikanusha kuwapo kwa migogoro kanisani hapo na kwamba, tukio hilo halihusiani na mgogoro wowote ndani ya Kanisa bali ni ugaidi.
Majeruhi aendelea vizuri
Hali ya majeruhi wa mlipuko wa bomu uliotokea kanisani hapo, Benadeta Alfred, imeelezwa kuendelea vizuri katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando alikolazwa. “Hali ya mgonjwa ni nzuri ukilinganisha na tulivyompokea kwani hata kuongea alikuwa hawezi, lakini hivi sasa anaweza kuongea japo kwa shida,” alisema Lema.
Chanzo:Mwananchi

TUKIO KATIKA PICHA: MAHABUSU AVUA NGUO NA KUBAKI UCHI ILI KESI YAKE ISIKILIZWE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Askari polisi wakiwalinda mahabusu wawili kati ya sita wanaotuhumiwa kwa kesi za mauaji, wakiwa wameng'ang'ania mlingoti wa Bendera ya Taifa huku mnoja akiwa mtupu mara baada ya kutoroka toka kwenye msafara wa mahabusu waliokuwa wakiingia mahakama ya wilaya ya Nyamagana na kisha mmoja wao kuvua nguo.
Inspector Henry akiwasihi mahabusu hao wawili wanaotuhumiwa kwa kesi za mauaji, kuachia mlingoti wa Bendera ya Taifa na kurudi kwenye chumba cha mahakama kwaajiri ya taratibu za kesi.
Inspector Veda (mwenye koti) akichukuwa maelezo ya Thobiasi Warioba (35), aliyeamua kuvua nguo zote na kubaki mtupu akiwa ameng'ang'ania mlingoti wa Bendera ya Taifa uliopo katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Nyamagana mkoa wa Mwanza, ambaye anakabiliwa na kesi ya mauaji Na. 32/2012. akiwa na mwenzake Hamis Ramadani (30).
Ushawishi ukiendelea.
Mahabusu Thobiasi Warioba (aliye mtupu) pamoja na mwenzake Hamis Ramadhani katu katu waking'ang'ania mlingoti wa bendera ya Taifa huku wakishinikiza kuzungumza na waandishi wa Habari.
Wananchi wamefurika viwanja vya mahakama.
Baada ya kuzungumza na waandishi wa habari mahabusu hao walikubali kurejea chumba cha Mahakama.
Nje ya Mahakama kuelekea lango kuu.
Wananchi wamefurika viwanja vya mahakama.
Mashuhuda.
Inspector Henry (shati la bahari) akiwa na Inspector Veda (mwenye koti) wakisikiliza hoja za  Thobiasi Warioba (35), aliyeamua kuvua nguo zote na kubaki mtupu akiwa ameng'ang'ania mlingoti wa Bendera ya Taifa uliopo katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Nyamagana mkoa wa Mwanza, ambaye anakabiliwa na kesi ya mauaji Na. 32/2012.
MAHABUSU wawili kati ya sita wanaotuhumiwa kwa kesi za mauaji, wameleta kizaazaa baada ya kujaribu kutoroka na kukimbilia kwenye mlingoti wa Bendera ya Taifa nakuing'ang'ania kisha kuvua nguo na mmoja wao kubaki mtupu.

Tukio hilo limetokea leo majira ya saa 4:00 asubuhi katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza, wakati mahabusu hao walipofikishwa kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi zao, lakini ghafla walipofika kwenye viwanja vya mahakama hiyo walitimua mbiyo kuelekea kwenye mlingoti wa Bendera hiyo ya Taifa na kuvua nguo.

Wananchi waliokuwa katika viwanja vya mahakamani hapo waliachwa midomo wazi na hali ya mshangao, mara baada ya mmoja kati ya hao wawili wakifanikiwa kuufikia mlingoti huo na kuvua nguo kisha kuanza kupiga kelele kwa kupaza sauti kudai haki itendeke.

 Tukio hilo pia lilishuhudiwa na watumishi wa Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Mwanzo, Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka ya jijini hapa (MWAUWASA), Askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), na taasisi zingine zilizo jirani na majengo ya mahakamani hapo na wananchi waliokuwa wakisubilia kesi zao kutajwa.

Mahabusu hao sita waliojaribu kutoroka na kuishia kudhibitiwa vyombo vya dola, walitajwa kwa majina kuwa ni Thobiasi Warioba (35), aliyeamua kuvua nguo zote na kubaki mtupu eneo la mlingoti wa Bendera ya Taifa, ambaye anakabiliwa na kesi ya mauaji Na. 32/2012.
 
Watuhumiwa wengine waliojaribu kutoroka ni Hamis Ramadani (30), Anthony Petro (35), Marwa Mwita (38), na Chacha Wangwe (35), na mwingine ambaye hakufahamika majina yake mara moja, wote wanakabiliwa na kesi ya Jinai Na. 215/2013  na walikamatwa tangu mwaka 2011.
 
Wakiwa katika viwanja vya mahakama hiyo baada ya kudhibitiwa na askari polisi, mmoja wa mahabusu hao walisikika wakisema: “Haiwezekani, tangu mwaka 2011 tulipokamatwa hadi sasa kesi zetu hazijasikilizwa. Wengine tumebambikiziwa kesi.  “Tunaomba haki zetu, polisi mnatuonea, vyombo vya habari tunaomba mtusaidie  tumekaa muda mrefu bila kusikilizwa na hatujui hatma yetu tangu 2011 tulipo kamatwa tumechoka kukaa mahabusu, tunaomba kesi zetu zisikilizwe”.

Baada ya malalamiko yao, ndipo askari  mmoja aliyejitambulisha kuwa ni Inspekta Henry akiwa na wenzake sita waliokuwa wakiwadhibiti wasikimbie na kuwahoji kuhusiana na madai yao, huku askari hao wakiwataka kuondoka katika mlingoti huo na kumtaka Warioba avae nguo ili waweze kuingia mahakamani.

“Pamoja na maamuzi yenu haya, lakini mtambue mnavunja sheria na hili ni kosa jingine la jinai, hivyo ni vema mkaondoka kwenye mlingoti huu na kuingia mahakamani. Malalamiko yenu tumeyasikia na yatashughulikiwa,” alisema Inspekta Henry.

Mmoja wa maofisa waandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, ambaye alikataa kutajwa jina lake, alidai ushahidi wa kesi za watuhumiwa hao bado haujakamilika, na kwamba kesi zao haziwezi kusikilizwa na mahakama ya wilaya kwani haina uwezo na badala yake zitatajwa tu kisha kuhamishiwa Mahakama Kuu.

“Bado hiyo ni Criminal Case (kesi ya mauaji) au PI Case hivyo Mahakama Kuu haiwezi kuzungumzia hilo kwa sasa kwa kuwa utaratibu wa mahakama kuu ikisha kuwa tayari huitwa ‘Criminary Session Case’, ambapo sasa hupangiwa namba ya kesi na Jaji wa kuisikiliza,”  alisema.
 

CHANZO:GSENGO BLOG

PICHA ZIKIONESHA NYUMBA NA JINSI MHUDUMU WA KANISA HUKO MWANZA ALIVYOLIPUKIWA NA BOMU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Damu zimetanda mbele ya lango la kuingilia Rest House ya Kanisa la KKKT Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria, mara baada ya tukio la kulipuka kwa bomu katika Ushirika wa Kanisa Kuu Imani jijini Mwanza.
Kwa ukaribu zaidi ni damu ya muhudumu wa rest house Bi. Bernadeta Alfred aliyelipukiwa na bomu lililowekwa kwenye kifurushi alichokifungua ili kubaini kilichokuwa ndani.
Hali tete.
Kishindo kikubwa kilitokea na kutoa sauti kubwa na moshi huku kikisambaza misumari mingi midogomidogo na kujeruhi vibaya mhudumu huyo hasa sehemu za miguuni na usoni.PICHA NA GSENGO BLOG

NDIKILO AITUPIA SSRA'KAA LA MOTO'

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo ametaka Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Jamii (SSRA) kutafuta ufumbuzi wa malalamiko ya wafanyakazi hasa utoaji wa mafao kwa wastaafu.
Pia, Ndikilo alisema SSRA inapaswa kuchukua changamoto zote zilizotolewa na wafanyakazi kwenye sherehe za Mei Mosi ambazo kimkoa zilifanyika viwanja vya CCM Kirumba, kwani wengi walidai baadhi ya mifuko kutoa mafao kidogo.
Akifungua mafunzo ya utoaji elimu kwa wafanyakazi wa halmshauri za Mkoa wa Mwanza jana kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mhandisi Evarist Ndikilo, Kaimu Katibu Tawala Mkoa, Warioba Sanya alisema changamoto za mifuko ya jamii zinapaswa kutafutiwa ufumbuzi kuondoa malalamiko ya wafanyakazi.
“Kumekuwa na malalamiko mengi ya wafanyakazi hasa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii, naomba SSRA mfanye jitihada kuhakikisha malalamiko hayo yanakwisha ili watumishi wanapostaafu wapate mafao bila matatizo,” alisema Ndikilo na kuongeza:
“Mifano hai tuliiona kwenye sherehe za wafanyakazi CCM Kirumba, kulikuwa na malalamiko mengi yanayohusu mifuko ya jamii ikiwamo kutoa mafao kidogo kwa wastaafu, hivyo naomba suala hilo litafutiwe ufumbuzi mapema.”
Ndikilo alisema kumekuwa na malalamiko ya utoaji mafao yanayotofautiana, jambo hilo linaibua kero kwa wafanyakazi hivyo ni vyema likatazamwa kwa undani.
“Kama mtafanya jambo hilo mtakuwa mmewasaidia, watumishi wote wa umma watanufaika na mifuko hiyo,” alisema Ndikilo.
Mwelimishaji kutoka SSRA, Sarah Kibonde alisema kumekuwa na tatizo la watu kutokujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii, jambo ambalo ni changamoto kwani idadi ya wanachama ni ndogo.
“Mpaka sasa takriban watu milioni 1.8 ndiyo wamejiunga na mifuko ya jamii, nia yetu ni kuhakikisha tunatoa huduma bora kwa Watanzania, hivyo sote tujiunge na mifuko hiyo kwa faida yetu,” alisema Kibonde.
Chanzo;Mwananchi

BOMU LALIPUKA ,LAJERUHI KANISANI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mlinzi wa kanisa hilo, Charles Mathayo alisema walisikia kishindo kikubwa cha mlipuko na baada ya muda mfupi wakasikia kelele za mhudumu huyo akiomba msaada

Mtu mmoja amejeruhiwa baada ya kulipukiwa na kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Ziwa Victoria, Makongoro Misheni, Mwanza.
Aliyejeruhiwa ni mhudumu wa nyumba ya wageni ya kanisa hilo, Benadeta Alfred (25) aliyekumbwa na mkasa huo juzi saa mbili usiku.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola alisema jana kwamba uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa ni bomu la kutengenezwa kienyeji linalojulikana kwa jina la IED na kwamba uchunguzi unaendelea kuwabaini walioliweka kanisani.
Mlowola alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa polisi wanapoona vitu ambavyo wanavitilia shaka ili uchunguzi wa kitaalamu ufanyike kabla ya kusababisha madhara.
Mlinzi wa kanisa hilo, Charles Mathayo alisema walisikia kishindo kikubwa cha mlipuko na baada ya muda mfupi wakasikia kelele za mhudumu huyo akiomba msaada.
Alisema walipofika eneo la tukio, walimkuta akiwa ameanguka huku akitokwa damu sehemu mbalimbali za mwili pembeni mwake kukiwa na vitu ambavyo alisema hakuvifahamu. Shuhuda mwingine, mwanafunzi wa Chuo cha Kompyuta kanisani hapo, Erina Emmanuel alisema walisikia mlipuko, baadaye wakasikia sauti ya mtu akiomba msaada, lakini kutokana na hofu walikimbia hawakwenda kumsaidia.
Lilifungwa kama zawadi
Kiongozi mmoja kanisani hapo ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema kitu hicho kilicholipuka kilikuwapo kanisani hapo tangu Ijumaa iliyopita, kikiwa kimewekwa juu ya makreti ya soda.
Alisema wahudumu walipuuza wakidhani ni mzigo wa mtu aliyekuwa ameusahau kutokana na jinsi ulivyokuwa umefungwa vizuri kwa karatasi za zawadi.
Alisema baada ya kuona bahasha hiyo imekaa muda mrefu bila kuchukuliwa, mhudumu huyo aliichukua kwa lengo la kuipeleka kwa uongozi wa kanisa.
Alipoushika, mzigo huo ulilipuka na kumjeruhi usoni na miguuni na kupelekwa Hospitali ya Bugando ambako amelazwa.
Hata hivyo, uongozi wa Hospitali ya Bugando uliwazuia waandishi wa habari kumwona majeruhi huyo.
Chanzo:Mwananchi

Uongozi wa Msitu wa Buhindi Sengerema wagawa madawati kwa shule za msingi

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Untitled
Afisa Elimu Msingi wilaya Sengerema Bw. Juma Mwajombe akikadhiwa madawati.
Na Daniel makaka, Sengerema.
WALIMU wakuu shule za msingi katika kata ya Bupandwa wilaya ya Sengerema mkoa wa  Mwanza wameombwa kutumia vyema madawati yaliyotolewa na uongozi wa  msitu wa Buhindi  kwa lengo la kusaidia kutatua tatizo la madawati katika shule hizo.
 Hayo yamesemwa  na Afisa Elimu ya msingi wilaya ya Sengerema Bw Juma Mwajombe katika sherehe za kukabidhiwa madawati hayo  iliyofanyika katika sherehe za Mei Mosi katika kata ya Bupandwa ambapo  uongozi wa msitu wa Buhindi ulikabidhi madawati 80 katika kata hiyo ambapo yatagawiwa katika shule zote za kata hiyo .
Untitled 1
Diwani wa kata ya  Bupandwa Bw. Masumbuko Bupamba akitoa shukurani baaada ya kukabidhiwa madawati.
Akikabidhi madawati hayo Meneja Msaidizi wa Msitu huo Bw Ernesti Madatta amesema kuwa msitu wa Buhindi umekuwa mstari wa mbele kusaidia jamii hiyo na  itaendelea kutoa misaada katika shule hizo ili kuleta usawa  kwa kuwa jamii hiyo inasaidia kulinda raslimali za msitu huo.
“madwati haya yamegharimu zaidi ya shilingi za kitanzania milioni tatu fedha taslimu na tutaendelea kutoa msaada kwenye jamii zinazotuzunguka,’ amesema Madatta.
Untitled 2
Meneja msaidizi msitu Buhindi  Bw. ERNEST MADATA.
 Bw, Madata aliongeza kuwa sambamba na kukabidhi  madawati hayo pia msitu huo unajenga kituo cha afya  katika kata hiyo pia jengo  la mama na mtoto katika zahanati ya Bupandwa ambapo kila moja itagharimu shilingi milioni sabini pia amewataka wananchi wa kata hiyo kushirikiana vema na msitu huo kuleta ushirikiano wa dhati miongoni mwao.
 Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo Bw Masumbuko Bupamba amemshukuru meneja huyo jinsi wanavyosaidia jamii hiyo na amewaomba waendelee na juhudi hizo za kusaidia jamii.
Untitled 44
Msitu wa Buhindi.
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mwanza Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa